ADDS

ADDS

Friday, 24 November 2017

DR SHIKA AIBUKIA KWENYE MAHAFALI NA UZINDUZI WA CHUO CHA SAYANSI YA AFYA KAHAMA,AAHIDI BILIONI 2 KWA WENYE NJAA YA ELIMU

Mkuu wa wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu leo amezidua rasmi chuo cha Sayansi ya afya kilichopo Mjini Kahama mkoani Shinyanga ambapo uzinduzi huo umeambatana na mahafali ya kwanza ya wahitimu wa mafunzo hayo katika chuo hicho.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya wilaya ya Kahama akiwemo Mtanzania aliyejizolea umaarufu hivi karibuni Dr. Louis Shika ambaye ameahidi kutoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kusomesha wanachuo ambao wazazi wao wameshindwa kuwalipia ada na wale ambao ni yatima wazazi wao wamefariki dunia.

Akizungumza katika hahafali hayo yaliyofanyika leo Alhamis Novemba 23,2017 Nkurlu aliwataka wahitimu wa fani mbalimbali wilayani Kahama kuwa waadilifu pale wanapopata nafasi ya kuihudumia jamii ili kukidhi matakwa ya kusomea fani hizo.

Nkurulu alisema baadhi ya wahitimu wa mafunzo mbali mbali wamekuwa wakishindwa kukidhi vigezo kutokana na kutokuwa na nia ya dhati ya kutekeleza wajibu wao kwa weledi na uadilifu.

Katika hatua nyingine Nkurlu alimwelezea Dr. Shika kuwa ni mtu wa pekee mwenye utulivu na usikivu na kuongeza kuwa wadau wengine waige kama alichofanya Dr. Shika katika kuinua elimu nchini.

Kivutio kikuu katika sherehe hizo akawa Dr. Louis Shika ambaye hivi karibuni amejingea umaarufu, alipojitokeza katika mnada wa nyumba za kifahari za Bilionea Saidi Lugumi zilizoko jijini Dar es salaam, kupitia msemo wake wa “(900 INAPENDEZA)” ambapo katika mahafali hayo ameahidi kutoa bilioni mbili kila mwaka kusomesha watoto yatima katika wilaya ya Kahama.

Dr. Shika alisema kuwa yeye ni mpenzi wa elimu na anapenda watu wote wapate elimu hivyo kupitia kampuni yake ya Lancefort atasaidia kusomesha wanachuo ambao wazazi wao wameshindwa kuwalipia ada na wale ambao ni yatima wazazi wao wamefariki.

Ahadi hiyo imekuja kufuatia risala ya chuo hicho iliyosomwa na Mkuu wa Chuo hicho na kuelezea changamoto wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na wazazi kushindwa kulipa ada pamoja na waanachuo wengine kushindwa kuhitimu mafunzo yao baada ya wazazi wao kufariki.

Dr. Shika alitoa wito kwa ofisi ya mkuu wa wilaya imuombe kusaidia kusomesha wanafunzi wasio na uwezo kwani kampuni yake inauwezo wa kusaidia watoto yatima katika wilaya ya Kahama hivyo milango iko wazi na yeye yuko tayari kusaidia watu wenye njaa ya elimu.

Akielezea kiwango atakachokitoa kusomesha wanachuo hao, Dr Shika amesema kuwa itakuwa ni dola milioni moja za Kimarekani sawa na Bilioni mbili ambazo atakuwa anazitoa kila mwaka kwa chuo hicho kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaopenda kusoma lakini wanashindwa kutokana na ukosefu wa ada.

Katika hatua nyingine Dr Shika aliwataka waandishi wa habari na mwenye chuo wasimuulize kuhusu msaada huo ndani ya wiki mbili kwani kwasasa hana pesa bali wasubiri mpaka mchakato wake wa kuhamisha fedha zake kutoka Urusi ukamilike.

Naye mkurugenzi wa chuo hicho Yonah Bakungile amesema kuwa kumekuwa na shida ya wanafunzi wanaomaliza vyuo vya uuguzi kutokuwa na maadili na kufikilia masirahi jambo ambalo limechangia kupoteza maana halisi ya masomo hayo.Aliwataka kuitumikia jamii bila ubaguzi na kuangalia maslahi binafsi ili kwenda sanjari na matakwa na viapo vya kada ya uuguzi duniani.

Aidha alisema baadhi ya Wahitimu wa vyuo vya uuguzi wanakosa uadilifu na kuweka mbele maslahi binafsi hulka inayopoteza maana halisi ya fani hiyo.

Katika Mahafali hayo ya kwanza, Jumla ya Wahitimu 33 wametunukiwa cheti cha Msingi katika Kozi ya Mwaka mmoja ya Ufamasia.

Chuo cha Sayansi ya Afya Kahama kilianzishwa mwaka 2016 kikitoa mafunzo katika fani za Ufamasia na Utabibu na kwamba jumla ya wanachuo 33 wamehitimu.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI

Wahitimu wakiingia ukumbini katika mahafali ya kwanza ya chuo hicho.Picha zote kwa hisani ya Kijukuu blog

Wahitimu wa Chuo cha Sayansi ya Afya wakiingia ukumbini kwa furaha wakiwa na furaha tele.

Wahitimu wakiwa ukumbini

Mkuu wa wilaya akiwa na mkurugenzi wa Chuo hicho pamoja na mke wa mkurugenzi Mrs Bakungile.

Mwanachuo wa Chuo cha Sayansi ya Afya akionyesha burudani ya kucheza nyimbo za utamaduni wa Kisukuma katika mahafali hayo.

Mwanachuo akiendelea kutoa burudani katika uzinduzi wa chuo hicho.

Meza kuu ikifuatilia kwa makini burudani ya nyimbo za asili katika mahafali hayo.Meza kuu ikifuatilia kwa makini burudani ya nyimbo za asili.Familia na ndugu wa Mkurugenzi wa Chuo hicho wakiwa katika sherehe hizo wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmiMkurugenzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya Ndugu Yonah Bakungile akitoa neno kwa wahitimu katika mahafali hayoWageni waalikwa pamoja na wazazi wakiwa katika sherehe za mahafali na uzinduzi wa chuo cha sayansi ya afyaMwenyekiti wa bodi ya shule akimkaribisha mkuu wa wilaya ya Kahama kutoa hotuba yake.Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akitoa hutuba kwa wazazi na wahitimu katika mahafali hayo.Dr. Shika akitoa neno kwenye mahafali hayoDr. Shika akishikana mkono na Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili NkurluDr. Shika akishikana mkono na mkurugenzi wa chuo hichoMgeni muhimu wa katika mahafali hayo Dr. Louis Shika akipeana mkono na wageni wa meza kuu baada ya kutoa neno lakeKikundi cha sanaa kutoka hospitali ya wilaya ya Kahama wakitoa burudani katika uzinduzi huo wa chuo

Burudani inaendeleaWahitimu wakiwa wameketi katika nafasi zao Mwenyekiti wa mtaa wa Nyasubi Leonard Mayala kulia akiwa na Dr Louis Shika katika sherehe hizoMkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akikakugua maabara ya kufundishia kwa vitendo katika Chuo hicho.

Mkuu wa wilaya ya Kahama akiendelea kupata maelekezo kuhusu elimu ya vitendo wanayoipata wanachuo katika chuo hicho.

Msafara wa mkuu wa wilaya ukikagua chumba cha Computer katika chuo hicho.

Elimu bora ni pamoja na mazingira bora ya kusomea na kufundishia,Hili ni moja ya darasa katika chuo cha Sayansi ya afya Kahama.

Masomo kwa vitendo,Hili ni moja ya darasa la kufundishia likiwa na vifaa vya kisasa vya kufundishia katika chuo hicho.

Masomo kwa Vitendo hiki ni chumba maalumu cha kufundishia kikiwa na mfano wa wodi ambapo wanafunzi wanafundishwa kwa vitendo namna ya kuhudumia wagonjwa wakiwa chuoni hapo.

Moja ya darasa la kufundishia katika chuo cha Sayansi ya afya kilichozinduliwa leo mjini Kahama.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mjini Kahama wakiwa katika sherehe hizo.

Mkuu wa wilaya ya Kahama akiendelea kutembelea vyumba katika chuo hicho

Wanachuo wa mwaka wa kwanza na wa pili wakiwa katika mahafali hayoWazazi wakiwa katika mahafali hayo

Picha zote kwa hisani ya Kijukuu blog


Wednesday, 22 November 2017

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA VIONGOZI WA KUU WA OFISI YA MAKAMU WA RAIS.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Joseph K. Malongo na Naibu Katibu Mkuu Bi. Butamo K. Philip ofisini kwake Ikulu, jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba (wa pili kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Joseph K. Malongo(kulia) na Naibu Katibu Mkuu Bi. Butamo K. Philip  (kushoto) ofisini kwake Ikulu, jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

Tuesday, 21 November 2017

NINI MAANA YA MAZINGIRAMazingira ni vitu vyote vinavyotuzunguka vyenye uhai na visivyo na uhai. Vitu vyenye uhai ni pamoja na mimea na wanyama na visivyo ni pamoja na uhai ni hewa, ardhi na maji

 Mazingira yanahusisha pia vitu vyote vinavyosaidia kuendelea kuwepo kwa maisha ya mwanadamu na viumbe wengine. Hivyo basi maisha ya viumbe hai wa kizazi kilichopo na kijacho kinategemea uwepo wa mausiano mazuri kati ya watu namazingira.

UWEKEZAJI USIOZINGATIA TARATIBU KATIKA KILIMO UNAANGAMIZA MISITU.
UWEKEZAJI katika mashamba makubwa na usiofuata taratibu, unachochea ufyekaji misitu na kuhatarisha ustawi wa misitu nchini, imefahamika.
Hofu hiyo inathibitishwa na yaliyotokea mkoani Lindi katika miaka ya hivi karibuni ambako ardhi iliyochukuliwa kutoka vijiji vinne wilayani Kilwa kwa ajili ya uwekezaji kwenye kilimo cha mibono ilikuwa ya misitu minene ya asili, ikiwa na miti mikubwa yenye thamani.
Wataalamu wa misitu wanaielezea hatua hiyo kutokuwa  rafiki kwa mazingira kwa sababu inachochea kupotea kwa misitu nchini.
Miongoni mwa miti iliyomo kwenye ardhi iliyotolewa kwa ajili ya uwekezaji kwenye kilimo cha mibono, kwa mujibu wa wakazi wa vijiji hivyo, ni pamoja na mninga, mpingo, mkangazi, msekeseke na mkongo.
Mti wa mninga unatajwa kutoa mbao zenye thamani zaidi katika soko la mbao nchini na duniani, kikubwa zikitumika kutengeneza samani. Kwa upande wa mpingo ni mti wenye kutumika na wenyeji wa mikoa ya Lindi na Mtwara kutengeneza vinyago, moja ya sanaa yenye thamani kubwa duniani.
Vijiji vilivyotoa ardhi yao kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha mibono wilayani Kilwa ni Mavuji, Migelegele, Liwiti na Nainokwe, vyote vikiwa katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Katika kile kinachonekana ulikuwa mkakati maalumu wa kufanikisha kampuni hiyo inapata ardhi hiyo kirahisi, upimaji ulifanyika pale mwekezaji alipofika kukabidhiwa ardhi aliyopewa. Kilichofanywa na vijiji ilikuwa kutenga maeneo tu kwa ajili ya matumizi mbali mbali.
Utafiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la Hakiardhi unaonyesha kuwa Kampuni ya Bioshape iliomba hekta 82,000 za ardhi katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Hata hivyo ilipatiwa hekta 34,000 ambapo walitumia hekta 400 tu za shamba la majaribio.
Mahojiano ya hivi karibuni kati ya waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini (JET) waliotembelea vijiji hivyo, yanaibua mkanganyiko kuhusu ukubwa halisi wa eneo lililotolewa na vijiji hivyo kwa kampuni hiyo ya Bioshape.
Wakati tafiti za wataalamu zinaonyesha ni hekta 34,000, serikali za vijiji wanataja takwimu chini ya hizo.
Mathalan, katika Kijiji cha Mavuji, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, Muhidini Ulambe anasema walitoka ekari 16,000 ambazo ni chini ya hekta 10,000. Eneo hilo awali lilikuwa ni msitu wa asili.
Afisa Mtendaji Kijiji cha Naikone, Abdallah Said Kigomba anasema wao walitoa ekari 16,000.89 nazo zikiwa chini ya hekta 10,000.
Pamoja na ekari 16,000 ambazo Kijiji cha Mavuji wanaeleza kutoa, pia kijiji hicho kilitoa hekta zake 1,000 kutumika na mwekezaji kama shamba la mfano.
Wananchi wafichwa mikataba
Katika hali yenye kutia shaka, hakuna hata kijiji kimoja chenye nakala ya  mkataba wenywe kuonyesha ardhi waliyoitoa kwa mwekezaji huyo. Kilichopo kwenye vijiji hivyo ni mkataba wa ahadi za mwekezaji kwa vijiji.
Sheria ya ardhi inaweka ukomo wa kiwango cha utoaji ardhi kwa kila ngazi ya uongozi ambapo kwa kijiji mwisho ni hekta 50, zaidi ya hapo hutolewa kwa idhini ya Rais baada ya wanakijiji kuridhia iwapo eneo wanalo.
Kilichofanyika kwa ardhi iliyochukuliwa kwenye vijiji hivyo vinne wilayani Kilwa, ni maafisa wa Serikali kuwashawishi wananchi kuwakubalia wawekezaji kuchukua eneo wanalolihitaji na wakaridhia wakiwa hawaelewi wanaridhia kuchukuliwa ardhi ya ukubwa gani.
Nakala za mikataba hiyo zinaonyesha kuwa mikataba iliandaliwa na Kampuni ya uwakili ya FK Law Chambers, Advocates na Kitengo cha sheria, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Vijiji vilipelekewa na viongozi wake kutakiwa kusaini tu.
“Tuliletewa mkataba kusaini tu, kati yetu na mwekezaji kuhusu masharti tuliyowapa, mkataba ulitengezwa na mwekezaji na halmashauri,” anasema Yusuf Mohamed, maarufu kama Tangi.
Tangi ndiye  aliyekuwepo wakati wa utoaji wa ardhi hiyo kwa mwekeji huyo wa ajili ya kilimo cha mibono akiwa kama mwenyekiti wa Kijiji.
Afisa Programu kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya HAKIARDHI, Joseph Chiombola, anaubainisha udhaifu huo kuwa unachangiwa zaidi na utaratibu wa wananchi au vijiji kusaini nyaraka kwa msukumo wa kupata pesa au ahadi.
“Tatizo la wananchi wengi ni kukubali kusaini nyaraka za fidia bila kusoma na kuelewa kilichomo kwenye nyaraka hizo,” anasema Chiombola ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Kiombola aliibainisha changamoto hiyo wakati akitoa mada kuhusu umiliki wa ardhi nchini kwa waandishi wa habari walio katika Mpango wa Ardhi yetu Ajenda Yetu unaotekelezwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Pwani na Lindi na kuratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwenye tovuti ya  https://www.tnrf.org/, Kampuni ya Bioshape Tanzania ambayo ni uzao wa Bioshape Holdings ya nchini Uholanzi, ilianzishwa nchini kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa ya mibono.
Hata hiyo, kampuni hiyo haikuwekeza kwenye kilimo hicho kama walivyoahidi kwa vijiji hivyo pamoja na Serikali.
Wavuna miti wakatelekeza mibono
Kijiji pekee walichoanzisha shughuli zao kati ya vinne walikopewa ardhi, ni Majivu ambako waliandaa vitalu vya mibono ambavyo hata hivyo inaelezwa kuwa walivitelekeza na hawakuwahi kuvuna.
Katika vijiji vilivyobakia, mwekezaji hakuwahi kufanya jambo lolote, ardhi aliyopewa ilibaki vile vile, wakati katika Kijiji cha Majivu walivuna miti yote mikubwa kwenye eneo walilopewa na kuliacha likiwa na miti midogo na vichaka tu.
Mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni hiyo, Jafari Mbudo anathibitisha mwekezaji huyo kuandaa vitalu kwenye shamba la mfano, lakini wakijihusisha zaidi na uvunaji mazao ya misitu.
“Dhumuni walilotueleza ilikuwa kulima mibono, walipanda katika shamba la mfano, lakini hawakuwahi kuvuna, kikubwa nilichokiona, walivuna miti na kupasua mbao, wakapakia kwenye containers,”  anasema Mbudo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mpingo Conservation and Development Initiative, Makala Jasper anasema shirika lao lilikuwa la kwanza kupiga kelele wakitoa tahadhari kuhusu kutoa maeneo ya misitu kwa ajili ya uwekeaji.
“Uwekezaji unaofyeka misitu na usiofata taratibu haufai, unaangamiza misitu,” anasema Jasper.
Shirika hilo lilishuku hadi Tathmini ya mazingira (EIA), kwamba ilikuwa ya kugushi na taratibu hazikufuatwa.
Jasper anabainisha kuwa iwapo EIA ingefanyika vizuri, ingebainika tokea mwanzo kuwa uwekezaji wao haukuwa wa manufaa.
Uwekezaji kwenye uvunaji mazao ya misitu ulikuwa mkubwa zaidi ikilinganishwa na kilimo chenyewe cha mibono ambayo ndiyo shughuli yao ya msingi (core business).
“Nguvu waliyoitumia kwenye kuvuna mazao ya misitu na waliyotumia kwenye kilimo cha mibono vilikuwa haviwiani,” anasema Jasper.
Baadhi ya wanavijiji walioajiriwa kwenye kampuni hiyo, wanafichua kuwa mwekezaji aliwekeza mitambo mikubwa ya kuvunia miti na kupasua mbao, wakati kwenye zao la mibono, vitalu vyake ni kama watu walikuwa wanacheza, hakukuwa na umakini wowote.

Sunday, 19 November 2017

JAFO ASITISHA MKATABA WA MKANDARASI WA BARABARA YA NAMELOK-SUNYA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA Bw.Victor Seif wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya kutoka Namelock hadi Sanya iliyopo Wilayani Kiteto Mkoani Manyara.Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Sunya katikaWilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.

Ujenzi unaoendelea wa Barabara ya Namelock hadi Sunya kwa kiwango cha Changarawe yenye urefu wa kilometa 88.1 zilizoko katika wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Seleman Jafo amesitisha mkataba wa Mkandarasi Maginga Business Holding Co. L.t.d aliyekuwa akijenga barabara kutoka Namelok hadi Lopeltes kwa kushindwa kumaliza ujenzi huo kwa wakati wilayani Kiteto , Mkoani Manyara.

Waziri Jafo amefikia hatua hiyo baada ya kukagua na kutoridhishwa na kazi inayofanywa na Mkandarasi huyo.

Jafo amemuagiza Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) kumpeleka mahakamani na kumfuta katika orodha ya wakandarasi , mkandarasi huyo kwa kutaka kuitapeli serikali.

Amesema kuwa mkandarasi huyo amekiuka makataba na kutaka kufanya utapeli kwa serikali kutokana kampuni yake kukosa wataalamu pamoja na vifaa vya kisasa kwajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo alitakiwa kujenga umbali wa kilomita 41.1 ndani ya miezi tisa lakini hadi sasa mkataba unaonyesha tayari amesha fanya kazi kwa miezi mitano na imebakia minne huku kazi ikiwa imefanyika kwa asilimia 7.

Amebainisha mkandarasi huyo katika kipindi cha miezi yake mitano alichoweza kufanya ni kusafisha eneo la kilomita 17 pekee na kushindwa kuifikia asilimia 50 ya mkataba wake.

Aidha,Waziri Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya kote nchini kusimamia miradi ya maendeleo nchini ili thamani ya fedha inayotolewa na Serikali iendane na thamani ya miradi inayotekelezwa nchini.

Jafo amesema kazi kuu ya Wakuu wa Mikoa nchini ni kusimamia maagizo yanayotolewa na serikali hasa katika suala zima la kusimamia maendeleo katika maeneo yao ili fedha zinazotolewa ziendane na kazi zinazotekelezwa katika jamii.

Kwa upande wake, Mtendaji mkuu wa Tarura Victor Seff, amesema kuwa maagizo ya serikali wameyachukua na watayafanyia kazi ili kuhakikisha kuwa fedha za serikali hazipotei kwa wakandarasi wababaishaji kama hao.

Saturday, 18 November 2017

BOT yatolea ufafanuzi taarifa ya kufungwa kwa benki ya Amana

 
RPC SIMON HAULE AFUNGA MAADHIMISHO YA WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI MKOA WA SHINYANGA MWAKA 2017

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule amefunga wiki ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoa wa Shinyanga yaliyoanza siku ya Jumatatu Novemba 13,2017 katika viwanja vya jeshi la Zimamoto mjini
Shinyanga.

Akizungumza leo Jumamosi Novemba 18,2017 wakati wa kufunga maadhimisho hayo, yenye kauli mbiu "Zuia ajali,Tii sheria,OkoaMaisha",Kamanda Haule aliwataka watumiaji wa barabara kuzingatia alama na michoro ya barabarani na watembea kwa miguu kuhakikisha wanapokuwa barabarani wanavuka katika maeneo yanayostahili ili kupunguza ajali zisizo za lazima.

Katika hatua nyingine aliwataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara kwa kushirikiana na serikali na kuhakikisha wanawakata baadhi ya watu wasio waaminifu wanaoiba miundombinu ya barabara.

“Naomba tushirikiane kuwafichua na kuwakamata watu wanaoiba miundombinu ya barabara,na tukiwakamata tuwafikishe katika vyombo vya sheria”,aliongeza Haule.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha akina mama kukaa mkao wa kiume wanapopanda pikipiki ama baiskeli badala ya kukaa upande upande ili kupunguza ajali za barabarani.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga,Anthony Masanzu alisema katika wiki hiyo ya nenda kwa usalama,wamefanikiwa kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda 184.

Alisema mbali na kutoa elimu kwa waendesha bodaboda na wananchi waliotembelea mabanda ya usalama barabarani pia walitembelea shule mbalimbali mjini Shinyanga ambazo zipo karibu na barabara.

“Tumetumia wiki hii kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa barabara ili kuhakikisha kuwa tunazuia ajali na kuokoa maisha yao”,aliongeza Masanzu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akizungumza wakati wa kufunga wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoa wa Shinyanga mwaka 2017-Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akisisitiza watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga,Anthony Masanzu akizungumza wakati wa kufunga wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoa wa Shinyanga

Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani mkoa wa Shinyanga,Wilson Majiji akizungumza wakati wa kufunga wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoa wa Shinyanga

Kwaya ya AICT Kambarage ikitoa burudani ya wimbo unaohusu masuala ya usalama barabarani

Wanafunzi wa shule ya msingi Town wakiimba wimbo  unaohusu  usalama barabaraniBurudani ya ngoma ya kucheza na nyoka ikiendelea

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akitoa vyeti kwa mmoja wa waendesha bodaboda (kati ya 184) waliopata mafunzo/elimu ya usalama barabarani wakati wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoa wa Shinyanga mwaka 2017.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog