Top Menu

TAMKO LA KUZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA TAMWA

8/31/2017 02:44:00 pm


Na Edda Sanga


Wanaharakati wenzangu, karibuni TAMWA, mahali adhimu ambapo tumeamua kuzindulia maadhimisho ya miaka 30 ya Chama Cha Wandishi Wa Habari Wanawake Tanzania.


Jina la TAMWA si geni masikioni mwa Watanzania walio wengi, ikizingatiwa hiki ni chama kikongwe cha wanahabari Tanzania ambacho mithili ya chombo baharini, kimehimili mawimbi, makubwa na madogo, mitikisiko na misukosuko ya hapa na pale, na bado kikaweza kuelea katika bahari tulivu. Itoshe kusema, tumetoka mbali.


Mimi mbele yenu ni mmoja wa waasisi wa Chama Cha TAMWA, kwa niaba ya wenzangu kumi na mmoja, tulio hai ni kumi, ambapo wawili wametangulia mbele za haki. Namshukuru Mungu ametujalia neema ya kuuona Mwaka uliotutunuku fursa ya kuanzisha Chama hiki, japokuwa tunazindua harakati za maadhimisho haya, tukiwa na takriban siku 78 kufikia kilele hapo tarehe 17 Novemba Mwaka huu.


Tungependa ndugu zetu, marafiki zetu, wadau wetu, Watanzania wenzetu mmoja mmoja na katika ujumla wenu, muungane nasi kufurahia fursa hii ya kuadhimisha siku hii muhimu ambayo katika historia ya kuwepo kwetu, tunahesabu mafanikio lukuki tuliyoyapata.


Moja ya mafanikio hayo ambayo ni vigumu kusahau ni ushawishi, kuzengea na kuzonga kuliko fanyika kwa ustadi mkubwa , tukiwa na wenzetu TGNP, TAWLA, MEWATA, WLAC, LHRC, CRC na mashirika mengine kama hamsini hivi tukitetea kubadilika kwa sera, na sheria kandamizi zinazomnyima haki mwanamke na mtoto, hasa mtoto wa kike. Furaha yetu ilikamilika , pale Mwaka 1998 tulipofanikiwa kuongea na wabunge, wakatuelewa na kuwazawadia Watanzania SHERIA YA MAKOSA YA KUJAMIIANA , maarufu kama SOSPA. Utakumbuka pia sheria hii iliboreshwa Mwaka 2005.


Uzuri wa sheria hii ya SOSPA, ni kwamba kwa mara ya kwanza, ilitamkwa wazi kuwa ukeketaji ni kosa la jinai, ikampa mtoto wa kike ulinzi wa kutofanyiwa ukatili akiwa chini ya umri wa miaka 18.

Huko Zanzibar, sheria ya spinster ambayo ilimtaka mtoto wa kike aliyepata mimba chini ya umri wa miaka 18 afukuzwe shule na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, wakati mwanaume aliachwa huru kutokana na kutokuwa na kifaa cha DNA, marekebisho yalifanyika katika sheria hiyo ambapo kifungo kwa mtoto wa kike kilifutwa na mwanamume aliyempa mimba anawajibika kutoa matunzo ya mtoto hadi atakapofika miaka 18.

Januari 2008 ulizinduliwa mpango wa kuboresha hali za wanawake kiuchumi na kijamii uitwao WEZA, ambao ulitekelezwa na shirika la CARE TANZANIA, kwa kushirikiana na TAMWA ZBR. Mpango huu uliangalia shehia ya Unguja Kusini, na Kaskazini Pemba kwa kuhusisha makundi 300 ya wanawake 6,000 ambao waliunda vikundi vya kuweka na kukopeshana kwa ajili ya uwekezaji katika miradi ya uzalishaji mali na kuongeza kipato kwa ajili ya ustawi wa jamii. Azma hii ni katika kuhalalisha usemi maarufu kwamba ukimwezesha mwanamke, umeiwezesha jamii.


Mafanikio zaidi ni pale kwa kushirikiana na wenzetu wanasheria, Mwaka 1999 sheria ya ardhi na sheria ya ardhi ya vijiji, iltoa fursa kwa wanawake kumiliki ardhi, na kwa mara ya kwanza, wanawake waliruhusiwa kushiriki katika kutoa suluhu ya migogoro ya ardhi.


TAMWA, kwa ujasiri mkubwa, ilivunja ukimya wa mauaji ya vikongwe yaliyokuwa yakiendelea Shinyanga na kufanikiwa kufanya suala hilo liwe ajenda ya kitaifa. Aidha kwa kutumia vyombo vya habari tukishirikiana na mashirika mengine, tulifanikiwa kuongeza idadi ya wanawake bungeni kutoka asili mia 20 mwaka 2000 hadi 36 mwaka 2005 na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tulimpata spika wa bunge mwanamke, Mama ANNE Semamba Makinda ambaye ametuwakilisha vizuri hadi alipostaafu.

Kama kuna kazi kubwa na ya kusifika imefanywa, na inaendelea kufanywa kwa ufadhili wa DANIDA toka mwaka 2012 ni katika GBV, ambapo TAMWA ikishiriana na CRC kituo cha usuluhishi na ushauri nasihi , na bila kusahau bang style ambayo kwa mfumo wake inafanana na kampeni. Mfumo huu tuliutumia sana TAMWA, ambapo vyombo vya habari vinatumika kwa wakati moja kuandikia na kutangaza suala moja kupitia angle tofauti tofauti kwa kipindi cha wiki, wakati mwingine hata zaidi.


Huu ni mkakati tuliouibua wakati tunapanga mipango iliyotupatia ushindi wa SOSPA. Matokeo yake ni makubwa , HAYANA KIFANI.


Kwa mtindo huo vile vile tumekemea na kuhamasisha jamii iachane na mila potofu, za kuwaoza kinguvu watoto wa kike katika umri mdogo kwa wanaume ambao wana umri mkubwa. Sifa nyingine kubwa kwa TAMWA, ni mafunzo ambayo tumeendesha kwa nyakati mbali mbali kwa wandishi wa habari ili waziandike kwa jicho la jinsia.


Tumepinga ukatili dhidi ya watoto, tumehamasisha wazazi na walezi wawapeleke watoto wa kike shuleni ili wapate elimu, maarifa na ujuzi vitakavyosaidia kuwapa mawanda mapana ya fursa zilizopo ili wafaidi Maisha yaliyo bora kwa ajili yao na watoto wao.


Hatimaye tumeelimisha, tumehamasisha na tutaendelea na harakati hizo tukiamini watoto wa kike na wakiume wakizifahamu haki zao za kijamii, kiafya na kiuchumi, wataweza kuzipigania na kuzitetea, na hivyo taifa letu kuondokana na umaskini ili maendeleo endelevu yatapatikane katika kipindi kifupi.

Wanaharakati wenzangu, TAMWA toka mwanzo iliamini sana katika kufanya utafiti kabla ya kushughulikia tatizo lolote lile. Kwa mfano, tuliona wengi wetu tumejengwa kuimba nyimbo za kikoloni kama vile London bridge is falling down au where are you going my pretty maid. Huu ni utamaduni wa wenzetu ambao waliuingiza katika lugha yao.


Baada ya kutafakari, tukaona haina mantiki sisi Watanzania na hasa watoto wetu kuendelea kuimba nyimbo zinazo upaisha utamaduni wa wenzetu wakati tuna nyimbo zetu nzuri zinazo akisi mandhari mazingira, hulka, malezi na mazoea yetu. Tunazielewa zinatuhusu na zina mantiki, nyimbo kama mabata madogo madogo yanaogelea katika shamba zuri la bustani, au maua mazuri yapendeza au kofia nyembamba nk .Tukamtafuta mwanamziki wetu , mdogo wake marehemu Patrick Balisidya ambaye alitutengenezea cassette nzima ya nyimbo za watoto ambazo tuliwapa RTD wakati huo wazitumie kuweka mahanjam katika vipindi vya watoto. Kwa Bahati mbaya cassette haipo lakini kitabu kipo. Vivyo hivyo, wakati huo, suala la madawa ya kulevya lilikuwapo japo si kwa ukubwa tunaoushuhudia leo.


Tulifanya utafiti na kuangalia kiini chake, madhara yake na kuandika machapisho kadhaa kuihadharisha jamii kuingia katika angamizo la kizazi cha sasa na kijacho kama hatutafanya kazi ya ziada kuweka sheria kali dhidi ya wauzaji na watumiaji wa madawa ya kulevya. Waswahili wanasema mwanzo wa makubwa ni madogo na pia kwamba hata mbuyu ulianza kama mchicha. Kwetu TAMWA tulikemea,


Tuliandika sana na kufanya vipindi kadhaa redioni. TV wakati huo ilikuwa Znz tu.


Baadhi ya machapisho hayo ni Sauti ya Siti, ambayo ni sauti ya wanawake. Tumekuza sana sauti za wanawake na watoto, kudai washirikishwe katika maendeleo ya nchi ili kero zao zitatuliwe na mchango wao uthaminiwe na kuheshimiwa, waweze kuishi Maisha yenye hadhi na yenye ustawi.


Haya ni baadhi tu ya mengi yaliyofanywa na TAMWA.


Wakati tunaendelea na harakati hizi, tukiwa na umri huu mkubwa wa miaka 30. tunawiwa kuchukua nafasi hii ya kipekee kabisa, kuwashukuru wote, hasa wandishi wa habari ambao mmetuwezesha kuwafikia watanzania kwa idadi kubwa kwa kipindi chote hiki. Kama usemi wa Misri unavyodhihiri wakati wakizungumzia umuhimu wa mto Nile kwa uhai wao, kwamba no Nile, no Egypt, na sisi TAMWA tunasema no media no TAMWA. Nadhani mnanielewa. Kupitia kwenu vyombo vya habari, uelewa wa jamii umeongezeka, utayari wao kukemea madhila haya tunauona, tunausikia na tunausoma.

Kwa ushahidi zaidi tena wa kisayansi, TAMWA, inafanya kazi na inaendelea kufanya kazi katika wilaya kumi kwa ufadhili wa DANIDA unaoitwa GEWE I & 2 toka Mwaka 2012. Wilaya hizo ni WETE, (PEMBA KASKAZINI ) UNGUJA MJINI MAGHARIBI,UNGUJA KUSINI, KISARAWE,NEWALA MTWARA,MVOMERO MOROGORO,LINDI VIJIJINI,RUANGWA LINDI, KINONDONI NA ILALA DSM. Wakati mradi unaanza, uelewa wa watu katika wilaya hizo ulikuwa 11% , baada ya miaka 2, utafiti uliofanywa ulionyesha ongezeko la 4% hadi kufikia 16%. Kwa jicho la haraka haraka tunaweza kusema asili mi anne ni ndogo sana lakini ni kubwa kwa kipindi kifupi cha miaka miwili kwani kadri tunavyoendelea kuhamasisha na kuwapa uelewa na mbinu za kuchukua hatua, tutaona mabadiliko makubwa zaidi. Nini siri ya mafanikio yetu?

Tunapenda pia kutamka wazi, kwamba kujitolea kwetu, nyakati zile kwa hali na mali, na ujasiri wetu kushughulikia masuala ambayo kijamii bado yalikuwa na hat leo tunaweza kusema yana ukakasi, kumetujengea uwezo wa kuendelea kutetea haki za wanawake na watoto katika mfumo wa kisayansi. Uwezo wa kuthubutu umekuwa nguzo madhubuti na yote tuliyofanya tuliyaamini na tulichukulia kazi hiyo kama wito kwa jamii. Sisi tumepata faida ya kuwa wandishi tuisaidie jamii kwa ujumla wake nayo ipaze sauti lakini zaidi tulilenga wale walio dhalili miongoni mwetu wakiwamo wanawake , walemavu na watoto.

HUKO TUENDAKO:


Masuala ya unyanyasaji , ukatili wa kijinsia bado yapo, na naweza kusema ukatili umepitiliza kiwango cha ubinadamu. Hata ukatili kwa watoto unazidi. Hapa nazungumzia ubakaji ulawiti, utumikishaji watoto katika mashamba, majumbani , kwenye madanguro, ukatili wanaofanyiwa watoto mitaani majumbani mwetu na ndugu zetu, marafiki zetu, wageni wetu na majirani pia.

Mengi ya matukio haya hayaripotiwi TAMWA inasikitishwa sana na jamii inayoishi karne ya 21 kukosa ujasiri wa kuripoti na zaidi kukosa uzalendo wa kutoa ushuhuda ili haki itendeke.Kama anavyosema Rais wetu Mh. Magufuli, rushwa inasababisha haki isitendeke na sote tunajua jinsi ambavyo baadhi ya wenye mamlaka wanavyopindisha sheria na kufanya mwenye haki aonekane mhalifu na mhalifu aonekane mwenye haki. Katika masuala ya ukatili na unyanyasaji rushwa imekithiri sana na ni kikwazo kikubwa sana katika kazi inayofanywa na TAMWA. Bila ushirikiano wa dhati kati ya familia zetu na vyombo vya dola, madaktari, walimu, majirani, madhehebu ya dini na serikali, matatizo haya ya kijamii hayawezi kuisha. Tutaendelea kujenga kizazi kiso maadili, kilichopondeka mioyo, kisichojiamini, kilichodhoofu kiafya, kiakili ambacho pia kitakuwa hakina mwelekeo.

Kituo cha usuluhishi na ushauri nasihi hapa TAMWA, kina uwezo wa kuwahudumia waathirika wa matatizo hayo, lakini hatuna mahali stahiki pa faragha ambapo mteja anaweza kujieleza kwa uwazi na kwa kujiamini.


TAMWA inataraji kuweka jitihada zaidi katika kuwasaidia vijana hasa katika kukabiliana na tatizo jipya la ukatili wa kijinsia utokanao na matumizi ya ya mitandao, yaani internet.


Tunawasaidia vijana ili wawe na mtazamo chanya katika Maisha yao na vizazi vyao. Wawe na mbinu za kutambua kupambana na ukatili huu mpya unaoendelea kukua kwa nguvu na kusambaa kwa haraka katika jamii yetu.

TAMWA, inataraji kuongeza mawasiliano ya karibu na vijana kupitia kurasa za face book, instagram twitter na kuboresha tovuti yetu ya www.tamwa.org ili iwe na taarifa nyingi zaidi za muhimu kwa jamii hasa kwa kizazi kipya cha dot.com.


Kwa mantiki hiyo, lengo la mkutano huu, ni kuzindua harambee ya kuchangisha fedha ili tupate kituo cha kuwasaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia ikiwezekana nchi nzima.


Aidha, tunaandaa kitabu kinacho akisi safari yetu ya miaka 30, yakiwemo mafanikio, matatizo, changamoto na mafunzo tuliyo pata katika kipindi chote hiki. Tuna mpango pia wa kutengeneza documentary ya kielectroniki itakayoelezea mengi zaidi kuhusu TAMWA.


Tuna imani kubwa Watanzania watatuchangia kwa hali na mali , ili haya tuliyopanga kufanya, yawezekane. Tunaomba tuwe sote katika mwelekeo wetu wa kutetea haki za binaadamu, kapinga ukatili dhidi ya wanawake, walemavu na watoto, ili TANZANIA yetu iwe na amani endelevu. 

ASANTE SANA KWA KUSIKILIZA.


NJIA ZA KUCHANGIA:

1. KWA NJIA YA TIGO PESA: -

Piga *150*01# OK

Chagua Lipia Bili

Ingiza Namba ya kampuni 606060

Weka Namba ya kumbukumbu 606060

Ingiza Kiasi kisha namba yako ya siri kukamilisha.

Jina la kampuni ni TAMWA

2. KWA NJIA YA BENKI:

Jina la Bank CRDB

Account namba: 01J2027600600

Jina la Account: TAMWA

Kwa maelezo zaidi tupigie simu namba 0222772681 au 0222771005 TAMWA.

Mahakama Yadai Agness Masogange Ana Kesi ya Kujibu

8/31/2017 02:40:00 pm
Msanii  Agnes Gerald maarufu Masogange,  anayetuhumiwa kutumia dawa za kulevya amekutwa na kesi ya kujibu.

Uamuzi huo umetolewa leo Agosti 31, na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Constatine Kakula, kufunga ushahidi wao kwa mashahidi watatu.

Mashahidi wa upande wa Jamhuri waliotoa ushahidi kwenye kesi hiyo ni Mkemia Elias Mulima kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye alipima sampuli ya mkojo na maofisa wawili wa polisi ambao walimpeleka Masogange kwa mkemia.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Masogange ambaye anatetewa na Wakili Reuben Simwanza, alidai atajitetea kwa njia ya kiapo na atakuwa na mashahidi watatu.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, mwaka huu, kwa ajili ya utetezi na kusema dhamana ya mshitakiwa inaendelea.

Masogange anadaiwa kati ya Februari 7 na 14 mwaka huu, maeneo  yasiyofahamika Dar es Salaam, alitumia dawa  aina ya heroin na Oxazepam.

SERIKALI YATUMIA BILIONI 85 KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI

8/31/2017 01:30:00 pmSerikali imesema kuwa imetumia shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu mjini Dodoma.

“Mfuko huu unaendelea kuhakikisha kuwa mawasiliano bora yanafika katika maeneo mengi nchini hususan vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara ambapo Takwimu zinabainisha kuwa, tayari mawasiliano   yamefikishwa kwenye kata 443, vijiji 1,939  kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Julai mwaka huu”, amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.

Ameongeza kuwa tayari Mfuko umetiliana saini mkataba na kampuni za simu za mkononi mwezi Agosti mwaka huu kuhakikisha kuwa zinapeleka mawasiliano kwenye kata nyingine 75 na vijiji 154.

Aidha, ametanabaisha kuwa hadi hivi sasa asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma ya mawasiliano nchini na kuongeza kuwa, Serikali kupitia mkataba wake na Kampuni ya Simu ya Halotel imefikisha mawasiliano kwenye jumla ya vijiji 3,069 kati ya vijiji 4,000 tangu walipoanza utekelezaji wa jukumu hilo mwezi Novemba, 2015 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso, amezitaka kampuni za simu za mkononi zinazopeleka mawasiliano vijijini na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ambazo zinapatiwa ruzuku na Serikali kuhakikisha kuwa zinatoa taarifa sahihi kwa Mfuko huo ikiwemo hatua zilizofikiwa za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji husika.

 Amewataka UCSAF kujitangaza na kuweka mabango yao kwenye minara yote nchini iliyojengwa kupitia ruzuku ya Serikali ili kuwawezesha wananchi kutambua uwajibikaji wa Serikali katika kufikisha mawasiliano kwa wananchi wake.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete, amesema kuwa Wizara kupitia UCSAF itahakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na mawasiliano kuendana na jukumu la msingi la Mfuko huo la kufikisha mawasiliano kwa wote.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Eng. Peter Ulanga, amewahakakikishia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuwa Taasisi yake itashirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakiki kazi zilizofanywa na kampuni za simu za mkononi za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji mbalimbali nchini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo katika kikao na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Kakoso na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara hiyo Eng. Angelina Madete. 
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu miradi ya maendeleo ya mawasiliano vijijini katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kasoso, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati hiyo katika kikao kilichowakutanisha na uongozi wa Wizara ya  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Edwin Ngonyani.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu maeneo ya vijijini yaliyofikiwa na mawasiliano katika kikao na Kamati hiyo mjini Dodoma. Kulia ni Mhe. Dua Nkurua na kushoto ni Mhe. Rita Kabati wajumbe wa Kamati hiyo.


RAIS DKT MAGUFULI ASITISHA UBOMOAJI WA NYUMBA 300 TUANGOMA JIJINI DAR LEO.

8/30/2017 03:50:00 pm

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda Wamesitisha zoezi la BOMOA BOMOA kwa Nyumba zaidi ya elfu kumi na saba (17, 000) zilizotangazwa KUBOMOLEWA na Baraza la Hifadhi ya Mazingira NEMC.

Hatua ya kusitisha zoezi hilo, Imekuja kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda kuzungumza na Mhe Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuhusiana na Sintofahamu ya bomoa bomoa hiyo ambayo amemueleza Mhe Rais Magufuli kuwa Taarifa za BOMOA BOMOA ya Nyumba elfu kumi na saba iliyotolewa HAIKUFIKA ofisini Kwake, Jambo ambalo ni tofauti na Taratibu za Utendaji kazi wa Serikali.

Mhe Makonda amesema, hata kama TAMKO hilo limetolewa na watumishi wa Mkoa mfano Wakurugenzi wa Manisapaa au Wakuu wa Wilaya walioko Chini ya Mamlaka ya Mkuu wa Mkoa LAZIMA Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ipate taarifa na iridhie bomoa bomoa hiyo, na pia hata kama Taarifa zimetoka Wizarani inapaswa taratibu za kimaandishi zifuatwe kwa kujulisha Ofisi ya Mkoa.

"haiwezekani mtu kutoa TAMKO la kuvunja Nyumba elfu kumi na saba bila Mkoa kujua, hilo HALIWEZEKANI" amesema Mhe Makonda.

Mhe Makonda amefafanua kuwa AMEONGEA na Mhe Rais Magufuli na Kumuuliza kama ana taarifa za zoezi la Ubomoaji wa Nyumba elfu kumi na saba ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda ALIMUELEZA Mhe Rais Magufuli kuwa HANA taarifa hizo za UBOMOAJI, zaidi Ubomoaji wa Nyumba zilizo kwenye Hifadhi ya Barabara ya kuanzia Ubungo kwenda KIMARA na MBEZI Ubomoaji unaofanywa kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya Morogoro, Ubomoaji wa Nyumba zilizo Jirani na Reli hususani ni zile zinazohusiana na Ujenzi wa Reli Mpya na ya Kisasa.

Kutokana na Sababu hizo, Mhe Makonda amesema Mhe Rais amesikitishwa na TAMKO hilo la kutaka KUBOMOLEWA kwa Nyumba zaidi ya elfu kumi na saba na ametoa pole kwa Wananchi waliokumbwa na TAHARUKI ya TAMKO hilo la Ubomoaji, na kusisitiza kuwa Mhe Rais, Dkt. John Pombe Magufuli HAKUCHAGULIWA kwa ajili ya KUBOMOA Nyumba za watu na kusisitiza kuwa anataka wananchi WANAOISHI katika maeneo HALALI kuachwa mana AMEPATA taarifa kuwa huenda ZOEZI hilo lingekwenda mbali zaidi mpaka kwa Wananchi WASIOHUSIKA.

Katika HATUA nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda AMEPIGA MARUFUKU zoezi lolote UBOMOAJI wa Nyumba pasipo Ofisi yake kupewa TAARIFA na kisha KURIDHIA Ubomoaji huo.

Mwisho, Mhe Paul Makonda AMEWATAKA wananchi na wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kuzingatia SHERIA na wasivamie maeneo au kuuziwa VIWANJA na Matapeli na pia AMEWATAKA wananchi kuchukua TAHADHARI hususani ni katika maeneo yote HATARISHI ambayo sio SALAMA kwa MAKAZI na kuwataka kila Mwananchi Mwenye Familia KUTAFUTA Salama kwa Maisha yake na ya Familia yake.

Mhe Makonda Pia ametoa OMBI Maalumu Kwa Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi la KUBORESHA mfumo wa Ardhi katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzisha mpango wa kuweka MAAFISA ARDHI katika KATA zote za Mkoa wa Dar es Salaam ambao watakuwa na JUKUMU la KUSIMAMIA, KURATIBU masuala yote ya Ardhi ngazi ya KATA hatua ambayo itasaidia kuondoa Migogoro na UTAPELI kwa Wananchi kuuziwa au kununua Ardhi katika maeneo ambayo HAYARUHUSIWI, ambapo amesema amepata wazo hilo kutokana na uzoefu aliopata akiwa Rais wa umoja wa Vyuo vikuu -TAHILISO ambapo alishirikiana na Bodi ya Mikopo kuanzisha mfumo wa kuwa na MAAFISAMikopo katika vyuo hatua iliyosababisha kuondoa kero ya wanafunzi kufuatilia Mikopo katika Ofisi za bodi ya Mikopo hatua ambayo imekuwa mwarobaini wa tatizo la kufuatilia Mikopo kwa wanafunzi, Mhe Makonda amesema atamwandikia OMBI hilo na kulifikisha Rasmi kwa Mhe Lukuvi ili amsaidie kulifikisha kwa Mhe Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili utekekezaji.

Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.


30/08/2017 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wananchi wa Tuangoma wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam  na kusitisha bomoa bomoa iliyokuwa ikiendelea katika eneo hilo. Pia  amewaomba kujiepusha na kujenga nyumba za kuishi katika maeneo hatarishi.


Baadhi ya wananchi wa Tuangoma Wilayani Temeke wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam leo (hayupo pichani),Mhe. Paul Makonda  mara baada ya kutembelea eneo lao na kuzungumza nao.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa amezungukwa na wananchi mbalimbali wa eneo la Tuangoma,akitembelea maeneo ambayo nyumba zake zilikuwa zikitarajiwa kukumbwa na zoezi  la bomoa bomoa.
Baadhi ya Nyumba ambazo zilitakiwa kubomolewa,ambapo kwa sasa hazitabolewa kufuatia agizo la Rais Dkt John Pombe Magufuli kusitisha zoezi hilo na kuwataka wahusika wafuate taratibu na sheria za Ardhi .


Muda wa mwisho wa kuwasilisha maombi ya mikopo sasa ni Septemba 11 badala ya Septemba 4

8/30/2017 01:08:00 pmBodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa wanafunzi kuwasilisha maombi ya mikopo.

Hatua hiyo imeelezwa inalenga kutoa nafasi kwa wanafunzi walioshindwa kufuata masharti kuyakamilisha.

Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru amesema muda huo umeongezwa hadi Septemba 11 badala ya Septemba 4.

"Tumesogeza mbele kwa siku saba zaidi ili walioshindwa kufuata vigezo wakati wa kujaza fomu wafanye hivyo," amesema.

Amesema hadi kufikia jana Agosti 29, wanafunzi waliojitokeza walikuwa 49,282 lakini ni 15,473 waliokamilisha maombi kwa njia ya mtandao

Rais Trump azuru maeneo yenye mafuriko

8/30/2017 06:58:00 am

Donald Trump na mkewe Melania wakiwasili Texas

Rais wa Marekani Donald Trump ameanza ziara ya kuizuru Texas wakati taifa lake likiendelea kukabiliana na dhoruba kali ambayo imevunja rekodi kwa kiwango kikubwa cha mvua katika siku chache zilizopita.

Katika eneo la Corpus Christi mahali ambako awali kulishuhudiwa dhoruba hiyo, aliwashukuru wafanyazi wa vitengo vya dharula ambao walikuwa wakikabiliana na mafuriko ambapo alielezwa mafanikio makubwa ya uokozi.

Naye gavana , Greg Abbott, amemtaka rais huyo kutambua changamoto kubwa zinazoukabili mji wa Texas. Huko mjini Houston, Mabwawa mawili yameanza kufurika , kumeshuhudiwa Kuongezeka kwa mafuriko makubwa .

Pia Meya Sylvester Turner amesema kwamba mji wake umeomba msaada wa dharula wa shirikisho la nyumba kwa watu wengine elfu kumi kupatiwa makazi ya dharura

Baraza la Usalama la UN laionya Korea Kaskazini

8/30/2017 06:54:00 am

Kombora la Korea kaskazini

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani kitendo cha Korea Kaskazini kwa kurusha kombora kupitia anga la japan, huku nchi hiyo ikithibitisha kutekeleza.


Taarifa iliyoandikwa na Marekani, haikutishia kuiwekea vikwazo vipya Korea kaskazini.

Lakini Baraza la Usalama limeitaka Korea Kaskazini kusitisha majaribio zaidi na kusitisha mpango wake wa nuklia.
Wanachama 15 wa Baraza hilo la Usalama wameitaka korea kaskazini kuchukua hatua za haraka kupunguza hali ya wasiwasi uliyopo.

Majeshi ya Korea kusini na Marekani yamekuwa yakifanya mazoezi ya pamoja karibu na mpaka wa Korea kaskazini, jambo ambalo Pyongyang inasema ni mazoezi yenye kulenga uvamizi wa kijeshi.


Chanzo bbc

MAGAZETI YA JUMATANO LEO AGOSTI 30,2017

8/30/2017 06:47:00 am
 

 
Designed By Arusha Publicity | Developed By Gadiola Emanuel